Bunge laidhinisha kutumwa kwa wanajeshi kusaidia polisi kudhibiti maandamano

Marion Bosire
1 Min Read

Bunge la taifa leo liliidhinisha kutumwa kwa wanajeshi wa KDF kusaidia maafisa wa polisi kurejesha utulivu katika maeneo ya nchi ambayo yatakumbwa na vurugu.

Mjadala huo uliwasilishwa bungeni na kiongozi wa walio wengi Kimani Ichung’wa ambapo wabunge walikubalia kutumwa kwa maafisa wa KDF katika sehemu mbali mbali kulingana na mahitaji.

Awali Spika wa bunge hilo Moses Wetangula alitangaza kwamba alikuwa amepokea ombi la kuratibisha bungeni kutumwa kwa maafisa hao nyanjani nchini kutoka kwa baraza la usalama la kitaifa kupitia kwa waziri wa ulinzi Aden Duale.

Wetangula vile vile alihimiza wabunge kuwa wenye utulivu wanapozungumzia mambo yanayoendelea kushughulikiwa bungeni wakikumbuka jukumu lao kuu la kuwakilisha wakenya bungeni.

Ichung’wa aliwataka wabunge kupitisha suala hilo ikitizamiwa hali iliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Jukumu kuu la wanajeshi wa KDF huwa ni kulinda mpaka ya Kenya ardhini na angani isiingiliwe na adui na iwapo wanahitajika kuhudumu ndani ya mipaka ya nchi ni lazima idhini itolewe na bunge.

Wabunge wanakwenda kwa mapumziko mafupi kuanzia leo Jumatano Juni 26, 2024 na watarejea Jumanne Julai 23, 2024.

Share This Article