Bunge laibua wasiwasi kuhusu maporomoko ya ardhi na mafuriko

Marion Bosire
2 Min Read

Kamati ya bunge kuhusu maendeleo ya kikanda imeibua wasiwasi kuhusiana na maporomoko ya ardhi na mafuriko yanayoshuhudiwa katika sehemu mbali mbali nchini.

Wakihutubia wanahabari katika majengo ya bunge jana, wanachama wa kamati hiyo walitaka hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha usaidizi wa kibinadamu kwa waathiriwa.

Walitaka pia hatua za muda mrefu zichukuliwe katika kuimarisha uwezo wa Kenya wa kujiandaa kwa majanga na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Lochakapong ambaye ni mbunge wa eneo la Sigor alidhihirisha huruma kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Majanga hayo yamesababisha vifo vya watu 34, kukosesha wengi makazi na kuharibi nyumba za makazi, shule, barabara na njia za kujipatia mapato.

Maeneo ambayo yameathiriwa na maporomoko kutokana na mvua kubwa ni pamoja na Chesongoch katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, Kimende kaunti ya Kiambu, Kamutungi kaunti ya Embu, Tinderet kaunti ya Nandi na Narok Kusini katika kaunti ya Narok.

Mafuriko yameripotiwa katika maeneo kama Tana River, Laikipia na eneo zima la ziwa Viktoria.

Kamati hiyi iliahidi kusimama na waathiriwa wakati huu mgumu huku ikiomba mashirika husika kuharakisha juhudi za kutoa usaidizi unaofaa.

Wabunge hao walihimiza wakenya kuzingatia tahadhari zinazotolewa ili kuhakikisha wanasalia salama kama vile kutovuka mito, barabara na madaraja yaliyofurika, kuhama kutoka maeneo ya milima na ya chini, kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa na kushirikiana na maafisa wanaotoa usaidizi.

Walitangaza kwamba bunge la taifa liko katika hatua za mwisho mwisho za kupitishia mswada wa usimamizi wa hatari ya majanga.

Mswada huo unalenga kutoa mfumo wa kisheria na kitaasisi wa kujiandaa kwa majanga, hatua za baada ya majanga na jinsi ya kurejelea hali ya kawaida.

Share This Article