Bunge la Tanzania lamtuza Rais Samia

Alipokezwa tuzo hiyo na Spika Tulia Ackson ambaye alielezea kwamba alifanya hivyo kwa niaba ya wabunge wote.

Marion Bosire
1 Min Read

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemkabidhi Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan tuzo maalumu kutokana na utendakazi wake katika mida wa miaka minne ya uongozi wake.

Hafla ya kumkabidhi tuzo hiyo iliandaliwa jana Mei 31,2025 katika majengo ya bunge Jijini Dodoma na kutekelezwa na Spika wa Bunge hilo kwa niaba ya Wabunge wengine.

Katika kukubali tuzo hiyo, Rais Samia alisema kwamba mafanikio yaliyopatikana nchini Tanzania wakati wa uongozi wake yanatokana na kutekelezwa kwa matakwa ya maendeleo na ustawi ya wananchi wa Tanzania.

Matakwa hayo yaliainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Akielezea shukrani zake kufuatia kupokea Tuzo hiyo, Rais Samia alisema anaichukulia kama ishara ya kuthamini kazi ya pamoja kati ya mihimili ya dola, viongozi wa Serikali na wananchi wote kwa jumla walioshirikiana kwa karibu.

Samia alipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya kuisimamia Serikali kupitia mijadala ya bajeti, kwa kupitisha sheria muhimu na kutoa ushauri kwa Serikali ambao umeongeza tija katika utendaji kazi katika ngazi zote.

Spika Tulia Ackson alimpongeza Rais Dkt. Samia kwa uongozi wake wa kipekee na kueleza kuwa tuzo hiyo ilitolewa kwa niaba ya Wabunge wote.

Share This Article