Ni afueni kwa Gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo, baada ya Maseneta kupiga kura Jumatano jioni kusitisha hoja ya kumtimua afisini.
Kwenye kikao hicho, Maseneta 38 walipiga kura kumnusuru Gavana huyo, huku maseneta wanne wakitaka hoja ya kumtimua iendelee.
Hapo awali, mawakili wa Gavana Nyaribo walipinga mashtaka yaliyowasilishwa na bunge la kaunti ya Nyamira, wakisema hayana msingi wowote.
Kulingana na mawakili hao, hoja ya kumtimua Gavana huyo ya Novemba 11,2025, haikuafikia vigezo vya kisheria na kikatiba ili kumuondoa gavana afisini.
Mawakili wa Nyaribo walisema azimio la bunge la kaunti halikutimiza masharti ya kisheria chini ya sehemu ya 18 ya katiba na sehemu ya 33 ya sheria za serikali za kaunti.
Aidha, walishikilia kuwa ni wawakilishi wadi 19 waliokuwa bungeni wakati wa upigaji kura wa kumtimua gavana huyo, na wala sio 23 jinsi ilivyowasilishwa kwenye bunge la Seneti, swala walilolitaja kuwa ulaghai.
Kabla ya upigaji kura, Maseneta walijadili hoja hiyo huku wengi wao wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha haki inatendewa Gavana Nyaribo, wawakilishi wadi na wakazi wa Nyamira kwa jumla