Bunduki 15 za aina ya AK 47 na mizunguko 77 ya risasi zimesalimishwa kwa polisi na wakaazi wa eneo la Kerio Valley.
Bunduki hizo zilisalimishwa kwa polisi kwa ushirikiano wa kamati za kiusalama katika kata za Ketut, Chemwonyo, Mon, Kiptumbur, Kibaimwa, Chechan, na Murukutwo.
Hatua hiyo inapiga jeki juhudi za polisi kuwapokonya bunduki rai katika eneo hilo linalokumbwa na utovu wa usalama unaosababishwa na wizi wa mifugo.
Idadi hiyo inafikisha jumla ya bunduki zilizosalimishwa kwa polisi kuwa 205 na mizunguko ya risasi 1,413.