Brown Mauzo kuwania uwakilishi wadi Kileleshwa

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa muziki nchini Kenya Fredrick Kilonzo Mutinda, maarufu kama Brown Mauzo ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa mwakilishi wa wadi ya Kileleshwa katika kaunti ya Nairobi.

Kupitia Insta Stories Brwon alisema, “Sauti ya watu wa Kileleshwa ndiyo imekuwa nguzo yangu. Kwa muda sasa nimeguswa na wengi wenu ambao wameniomba niwanie wakilishi wadi”.

Mauzo aliendelea kutangaza nia yake akisema amejitolea kuhakikisha mustakabali bora wa Kileleshwa, “Ni kwa furaha kubwa na kujitolea kwa dhati kwa mustakabali wetu bora ninatangaza kuwania wakilishi wa Kileleshwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027”.

Alimalizia kwa kuhakikishia wakazi wa wadi hiyo ya Nairobi kwamba yuko tayari kushirikiana nao kuwahudumia huku akiwashukuru kwa kummotisha na kumwamini.

Brown alizaliwa huko Mombasa na alikuwa anapenda muziki tangu utotoni. Lakini alipata umaarufu mwaka 2007 kupitia muziki wake wenye mashiko na wa mtindo wa Bongo toka Tanzania.

Wadhifa huo wa mwakilishi wa wadi ya Kileleshwa kwa sasa unashikiliwa na mwanablogu Robert Alai Onyango wa chama cha ODM.

Share This Article