Robert Kyagulanyi au ukipenda Bobi Wine, kiongozi wa chama cha upinzani cha NUP nchini Uganda yuko katika hatari ya kufungiwa nje ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Hii ni baada ya chama hicho cha National Unity Platform – NUP kugundua jana Ijumaa kwamba mwaniaji huyo wa Urais huenda akapigwa marufuku kushiriki uchaguzi huo kutokana na sintofahamu ya saini za wanaomuunga mkono.
Katibu mkuu wa chama hicho David Lewis Rubongoya aliambia wanahabari jana alasiri kwamba Bobi anakabiliwa na hali hii kutokana na kutotimiza masharti yaliyowekwa.
Rubongoya alielezea kwamba tume ya uchaguzi ya Uganda ilifahamisha chama hicho kwamba bado hakijatoa orodha ya majina na saini za wapiga kura vitu ambavyo vinahitajika kabla ya kuidhinishwa kuwania Urais.
Madai hayo yanajiri siku chache tu kabla ya kufungwa kwa kipindi cha uteuzi wa wawaniaji na limesababisha tumbo joto kati ya wafuasi wa Bobi Wine.
Katibu mkuu alielezea kwamba wamekuwa wakiomba kufahamishwa na tume ya uchaguzi kuhusu saini zilizowasilishwa kwa wiki kadhaa lakini jibu walilipata jana tu kwamba idadi iliyopo haitoshi.
Uganda inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwezi Januari mwakani na tayari Bobi Wne alikuwa amechapisha kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii ujumbe kwamba uteuzi wake ungeidhinishwa Jumanne Septemba 23, 2025.
Tayari Rais Museveni na wawaniaji wengine wameidhinishwa kuwania Urais.