Mwanasiasa wa Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine (jina analotumia katika muziki) amekiri kwamba amewahi kuwaza kuhusu kuacha nafasi yake kama kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda.
Akizungumza katika kipindi cha kwanza cha jukwaa jipya la mtandaoni la chama chake cha National Unity Platform – NUP, mwanasiasa huyo alikiri kwamba mara kadhaa tangu aingie kwenye siasa mwaka 2017, amefikiria kuondokea.
Wine alielezea kwamba kitu ambacho humpa motisha sio ujasiri bali ni hisia ya kukata tamaa kwa kujitoa bila kurudi nyuma na wajibu mkubwa alionao kwa wafuasi wake.
“Ndiyo. Nimewahi kufikiria kuacha mara nyingi sana,” Bobi Wine alifichua akiongeza, “Wakati mwingine najiuliza, niliingiaje huku? Kwa sababu kiukweli sikuwa nimepanga kujihusisha na haya yote.”
Bobi Wine, ambaye ni msanii mashuhuri wa muziki na mwanaharakati wa kijamii aliyekuwa akijulikana kama “Rais wa mitaa” aliingia kwa mara ya kwanza kwenye siasa mwaka 2017 alipopata ushindi katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa eneo la Kyadondo Mashariki akiwa mgombea huru.
Alitafakari kuhusu hatua hiyo ya mwanzo akisema, “Ilikuwa jambo moja lililosababisha jingine, kulikuwa na hasira na nikaketi na Nubian na marafiki wengine tukasema, hebu tuwape changamoto hawa watu na kupeleka ghetto bungeni.”
Baada ya kuhudumu kama mbunge, Wine aliamua kujitosa kwenye ulingo wa kuwania Urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 ambapo alishindwa na Rais Yoweri Museveni wa chama cha NRM.
Msanii huyo anawania wadhifa huo wa juu kabisa nchini Uganda kwenye uchaguzi mkuu wa Januari 2026 ambapo yeye ndiye mpinzani mkuu wa Rais Museveni.