Mwanamuziki wa Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ametoa kibao kipya baada ya mapumziko ya miaka miwili hivi.
Wimbo huo uitwao “Not Your Enemy” ni ushirikiano kati ya Wine, Nubian Li na King Saha na kulingana na maelezo chini ya video yake kwenye YouTube, unaangazia kuhamasisha umma kwamba wao sio maaduni.
“Ukumbusho kwamba maadui wa kweli sio sisi kwa sisi bali ni mifumo ambayo inatukwamisha chini” yaliendelea kusema maelezo hayo.
Katika wimbo huo wasanii hao wanahimiza upendo, haki na mshikamano.
Awali, Bobi Wine alikuwa amechapisha picha inayomwonyesha akiwa studioni na wanamuziki wenza Nubian Li, King Saha pamoja na mtayarishaji muziki Paddyman.
Chini ya picha hiyo Wine aliandika, “Wakati maneno yanapungukiwa, muziki unazungumza”. Nubian Li naye aliongeza, “Mtafahamu hivi karibuni”.
Maneno ya wawili hao yalichangamsha mashabiki wao na kupandisha hamu ya kusikiliza wimbo uliokuwa ukiandaliwa.
Mara ya mwisho Bobby Wine ambaye pia ni mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda alitoa wimbo mpya ni mwaka 2023, wimbo alioshirikisha Nubian Li, Zex Bilangilangi, Feffe Bussi na Sizzaman.
Bobi Wine na Nubian Li wameshirikiana kwenye nyimbo nyingi za awali na hii ndio mara ya kwanza anamshirikisha King Saha.