Bobi Wine asema hakuchangia ufanisi wa kakake

Anasema kakake Dax Vibez alitia bidii ndiposa ameafikia ufanisi kama mwanamuziki.

Marion Bosire
2 Min Read
Bobi Wine na Dax Vibez

Mwanamuziki wa Uganda Bobi Wine amesema kwamba kamwe hakuchangia katika ufanisi wa kakake mdogo Dax Vibez kama mwanamuziki.

Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Sentamu amesema haya wakati ambapo Vibez kwa jina kamili Ivan Bugembe Sentamu, ameandaa tamasha lake kwa jina “All White Concert”.

Akizungumzia onyesho hilo la Agosti 29, 2025, lililofanikiwa pakubwa, Bobi Wine alijivunia safari ya kakake mdogo, akifafanua kwamba kukua kwake na kuafikia umaarufu kunatokana na bidii na kujitolea kwake.

Bobi Wine alisisitiza kwamba Dax Vibez hajasaidiwa na ushawishi wa ndugu zake ambao pia ni maarufu.

Mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Uganda alipongeza ndugu zake wakubwa Fred Nyanzi na Eddy Yawe, kwa kumuongoza akiwa kijana jukumu alilotekeleza kwa ndugu zake wadogo ambao ni Banjo Man, Micky Wine na Dax Vibez.

Hata hivyo anakanusha dhana kwamba maelekezo yake yalimwezesha Vibez kuafikia ufanisi kwani angeamua kuwa mvivu kwa sababu ana ndugu ambao wana umaarufu.

“Lakini aliamua kutia bidii katika kazi yake, akajiondoa kwangu.” Alisema Bobi Wine akiongeza kwamba Dax Vibez alichagua kujitafuta na kujiundia njia yake mwenyewe hatua ambayo anaamini ilisababisha aheshimiwe na umma.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya tamasha la Dax Vibez la “All White Concert” lililoandaliwa katika viwanja vya UMA na kulingana naye, lilifanikiwa akitaja mwezi Agosti kuwa wenye mafanikio kwake.

Share This Article