Bobi Wine aonya wanamuziki wanaoimba maneno machafu

Kulingana naye wasanii kama hao wako katika hatari ya kusahaulika baada ya miaka michache.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda ambaye pia ni mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ameonya wasanii ambao hutumia maneno machafu kwenye nyimbo zao.

Wine ana hofu kwamba wanamuziki wa siku hizi ambao wamechagua kutumia maneno machafu kwenye muziki wao wako katika hatari ya kusahaulika haraka.

“Inazua wasiwasi na sina uhakika iwapo wasanii wa sasa watajivunia maneno ya nyimbo zao kesho, watoto wao watakapoamua kuzisikiliza miaka 10 au 20 kutoka sasa.” Alishangaa Bobi Wine.

Aliongeza kwamba hali hiyo ni hatari sana kwao kwani wamejiweka katika hatarika ya kutokumbukwa na kutotambulika katika siku zijazo.

Hata hivyo alifafanua kwamba sio wasanii wa sasa pekee lakini kila kizazi cha wanamuziki kina wasanii wanaochagua kutumia maneno machafu na huwa wanaishia pabaya.

“Unajua ina maana gani wakati watu hawatakumbuka kizazi chako lakini wanatambua kizazi kilichotangulia chako?” Aliuliza Wine akiendelea kwa kutoa mfano wa wasanii wa kizazi chake.

Ushauri wake kwa wasanii wa sasa ni kufanya mambo na kurekodi miziki ambayo itawapa majivuno hata baada ya miaka kadhaa.

Share This Article