Mwanamuziki wa Tanzania William Nicholaus Lyimo, maarufu kama Billnass amezindua tamasha ambalo linalenga vyuo ambalo amelipa jina “Chuo kwa chuo”.
Akizungumza na wanahabari leo katika kikao kwenye hoteli ya Miramont huko Sinza Mori, Billnass alielezea kwamba yeye pamoja na wasanii anaoshirikiana nao, watazunguka vyuo mbali mbali nchini Tanzania.
Kando na burudani ya muziki, Billnass alisema wanafunzi wa vyuo vikuu watahusishwa kwenye shughuli kama vile majadiliano, michezo na hata kuelimishwa na kuhamasishwa kuhusu masuala mbali mbali.
Billnass amesema alichochewa kuandaa tamasha hilo na haja ya kurudisha fadhila kwa wanachuo kutokana na jinsi walivyojitoa kumsaidia wakati alikuwa akianza muziki.
Chuo kwa chuo inaanza rasmi tarehe 25 mwezi huu na chuo cha kwanza ni T I A yaani Tanzania Institute of Accountancy ambapo atakuwa na wasanii kama Whozu, Kusah, Chino Kidd na wengine.
Billnass amehimiza wanafunzi wa vyuo mbali mbali wafuatilie ukurasa wake wa Instagram kufahamu zamu yao huku akiwahimiza pia watoe maoni ya mahali ambapo wanataka apeleke tamasha hilo.
Msanii huyo anaonekana kufuata nyayo za mke wake Nandy ambaye pia ni mwanamuziki kwa kuandaa tamasha. Nandy amekuwa akiendesha tamasha lake kwa muda sasa kwa jina Nandy Festival.