Billnass aendeleza ufafanuzi wa maovu ya tasnia

Amemtaja Michael Mlingwa A.K.A Mx Carter anayehusika na usambazaji wa kazi zake za muziki kidijitali akisema mara nyingi huwa hapatiwi pesa zinazotokana na mauzo.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Tanzania Billnass ameendeleza ufafanuzi kuhusu maovu aliyotaja awali yaliyo kwenye tasnia zinazojikita katika talanta na ambazo huletea mtu umaarufu.

“Juzi niliandika waraka kuhusu vitu vingi vilivyomo kwenye upande wa pili wa tasnia na sanaa zetu, lengo sio kuwavunja moyo au kuwatisha Watu Wapya au Vijana wenye ndoto ya Kuingia Kwenye Tasnia,” aliandika Billnass.

Alisema lengo lake ni “kuwakumbusha na kuwaandaa kukabiliana na ulimwengu wa kweli” huku akiwahimiza wawe wakiomba Mungu ili awape roho za kustahimili na nguvu za kukabiliana.

Billnass ameahidi kuanisha mambo kadhaa aliyoyataja kwenye chapisho lake la awali akichagua kuanza na dhuluma za wadau kama kampuni za muziki, mameneja, watangazaji wa kazi za sanaa, wamiliki wa vyombo vya habari na kampuni za usambazaji.

Msanii huyo amemtaja Michael Mlingwa A.K.A Mx Carter mmiliki wa kampuni ya Slide Digital anayehusika na usambazaji wa kazi zake za muziki akisema mara nyingi huwa hapatiwi pesa zinazotokana na mauzo.

“Unaweza ukamiini wimbo mkubwa Kama Puuh sijawahi kupata hata senti moja ya mauzo yake upande wa digital na hata unapofika wakati wa kupata stahiki zangu nakua naomba au kubembeleza na kuna makubaliano kisheria” aliandika Billnass.

Msanii huyo amesema kilio chake ni kimoja tu na kwa sababu amefungua ukurasa wa kupaaza sauti, huenda wasanii wengine wengi wakajitokeza kulalamika kuhusu Michael Mlingwa.

“Hiyo ni moja nitarudi kuelezea mengi yanayofanywa na watu kama Mx Carter na washirika wao…” alimalizia Billnass katika kile kinachochukuliwa kuwa hatua nzuri ya kufichua maovu ya tasnia.

Share This Article