Bien aandikisha historia, Wakenya wajivuna

Alihojiwa kwenye kipindi maarufu cha redio cha Marekani ambapo amekuwa Mkenya wa kwanza.

Marion Bosire
1 Min Read

Msanii wa muziki wa asili ya Kenya Bien Aime Barasa ameandikisha historia ya kuwa Mkenya wa kwanza na msanii wa kwanza wa Afrika Mashariki kuwahi kuhojiwa kwenye kipindi maarufu cha redio cha Marekani ‘The Breakfast Club’.

Hatua hiyo imewafanya Wakenya wengi wafurahi mitandaoni.

Kipindi hicho kinaongozwa na DJ Envy, Charlamagne Tha God, Jess Hilarious na Loren Lorosa na huwa kinahoji watu maarufu ulimwenguni huku watangazaji hao wakisifiwa kwa mbinu zao za mahojiano.

Barasa yuko nchini Marekani kwa ajili ya ziara yake ya kikazi ya majimbo 10, tamasha ambazo tiketi zake zinaripotiwa kununuliwa kwa wingi.

Ziara hiyo ilianza Mei 14 huko Washington DC katika ukumbi wa Howard na ametumbuiza kwingine kama vile, Boston,New York, Atlanta, Minneapolis kati ya maeneo mengine.

Baada ya Marekani anatarajiwa kuelekea Ulaya ambako atakuwa na matamasha sita mwezi Julai.

Katika mahojiano hayo, Bien ambaye aliamua kuwa msanii huru baada ya kundi la muziki la Sauti Sol kusambaratika, alifichua kwamba mke wake Chiki Kuruka ambaye ni mcheza densi na mwalimu wa densi ndiye meneja wake.

Kuhusu utamaduni wa ndoa za wake wengi, Barasa aliambia watangazaji hao kwamba hata ingawa katiba ya Kenya inaruhusu, yeye mwenyewe hataki wake zaidi.

Share This Article