Besigye na Lutale kuendelea kuzuiliwa hata baada ya uamuzi wa mahakama ya upeo

Mahakama ya upeo iliamua kwamba raia hawafai kushughulikiwa na mahakama za kijeshi lakini jeshi litaendelezakesi hiyo na kwamba hawataachiliwa.

Marion Bosire
2 Min Read
kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye.

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye na msaidizi wake Haji Obeid Lutale wataendelea kuzuiliwa kwenye gereza la kijeshi hata baada ya uamuzi wa mahakama ya upeo.

Mahakama hiyo ya upeo ilikuwa imeamua kwamba mahakama za kijeshi hazina mamlaka ya kuwafunguliwa kesi watu ambao sio wanajeshi.

Lakini furaha ya wafuasi wa wawili hao ilikatizwa Jumamosi, kufuatia taarifa iliyotolewa na afisa mmoja mkuu wa jeshi la Uganda.

Kanali Chris Magezi alitangaza kwamba Kizza Besigye hataachiliwa kufuatia uamuzi wa mahakama ya upeo na kwamba kesi yake itaendelea kwenye mahakama ya kijeshi huku Rais Yoweri Museveni akitoa uamuzi wa mwisho.

Rais Museveni amepinga vikali uamuzi wa mahakama ya upeo ambao unazuia raia kupelekwa kwenye mahakama za kijeshi akisema ulikuwa uamuzi mbaya.

Katika taarifa Jumamosi, Museveni alitetea jukumu la mahakama ya kijeshi katika kushughulikia kesi za raia wanaopatikana na makosa yanayohusiana na silaha hususan bunduki.

Museveni aliendelea kusema kwenye taarifa yake kwamba mahakama za kijeshi zilisaidia kurejesha nidhamu huko Karamoja na hivyo hawawezi kuacha kuzitumia kwani ni vyombo muhimu vya uthabiti.

“Mahakimu ambao ni raia walikuwa wanaogopa hata kufika Karamoja. Mahakama za kijeshi zilituliza Karamoja na kuokoa maelfu ya vijana wapiganaji maarufu kama Karachunas ambao sasa wamezuiliwa kwenye magereza” alisema Museveni.

Kulingana naye, iwapo vijana hao hawangezuiliwa labda sasa wangekuwa wamefariki kufuatia makabiliano na wanajeshi.

“Hata hivyo, nchi haitawaliwi ma majaji. Inatawaliwa na watu wote wa Uganda, ambao wametimiza umri wa kupiga kura.” alisema kiongozi huyo wa Uganda.

Aliongeza kusema kwamba katika suala la katiba na sheria nyingine, watu wa Uganda wanajitawala kupitia kura za maoni au marekebisho ya katiba au marekebisho ya sheria kupitia bunge.

Share This Article