Dadake marehemu waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, Beryl Achieng Odinga, alizikwa jana Jumamosi, Disemba 6, 2025, nyumbani kwao huko Kang’o Ka Jaramogi, Bondo.
Mazishi hayo yalivuta mamia ya waombolezaji, wakiwemo familia, marafiki na viongozi wa kitaifa, ambao walikusanyika kuenzi maisha na urithi wake, huku kanisa katoliki likiongoza hafla hiyo.
Beryl alifariki Jumanne, Novemba 25, 2025, wiki chache baada ya kifo cha kakake, Raila Odinga. Ameacha watoto wake Ami, Auma, Chizi na Taurai.
Beryl alikuwa mtaalamu mashuhuri, akihudumu kama karani wa Jiji wa kwanza mweusi wa eneo la Mutare, nchini Zimbabwe, na baadaye kama Mwenyekiti wa Kampuni ya Maji na Mifereji ya Nairobi.
Mama Ida Odinga, shemeji yake Beryl, alizungumza kuhusu kumbukumbu zake binafsi za Beryl, akisisitiza kuhusu ukarimu wake na utu wake wa uchangamfu.
“Nilikutana na Beryl kwa mara ya kwanza nilipokuwa Chuo Kikuu cha Nairobi. Beryl alikuja nikiwa mwaka wa tatu” Ida alisema akiongeza kwamba alikuwa msichana mrembo, mwenye ufasaha na mwenye raha.
Ida alieleza kwamba Beryl alikuwa amerudi Kenya kutoka Zimbabwe na alikuwa akifanya kazi Nairobi wakati afya yake ilianza kudhoofika.
Alisema alienda kumwona hospitalini ambapo hakuweza kuzungumza na alikuwa na vifaa vingi vya matibabu, jambo lililomhuzunisha sana Ida.
Ida alibainisha kwamba kumwona Beryl katika hali hiyo kulimshawishi mara moja kumkataza Raila kwenda hospitalini, akisema aliogopa athari za kihisia ambazo zingempata, ikizingatiwa ukaribu wa pekee waliokuwa nao.
Wakati Raila baadaye alisafiri kwenda India kutibiwa, ambako hatimaye alifariki, Ida alielekeza wanafamilia kutomwambia Beryl akieleza kuwa alitaka kumlinda asipate msongo wa mawazo katika kipindi chake kigumu kiafya.
Ida alisema kwamba licha ya jitihada zake, taarifa za kifo cha Raila hatimaye zilimfikia Beryl, jambo ambalo anaamini liliongeza mashaka ya kihisia katika siku zake za mwisho.
Ida alisisitiza kuwa familia haijapata nafasi ya kumwomboleza Raila kabla ya kukabiliwa na kifo cha Beryl, akibainisha kwamba misiba hiyo miwili mfululizo imetikisa sana ukoo wa Odinga.