Benki Kuu ya Tanzania yakanusha uwezekano wa udukuzi

Marion Bosire
2 Min Read
Emmanuel Mpawe Tutuba, Gavana, Benki Kuu ya Tanzania

Benki Kuu ya Tanzania yaani Bank of Tanzania – BOT, imekanusha madai ya uwezekano wa kudukuliwa kwa mifumo yake ya malipo na akaunti za amana katika benki na taasisi za fedha nchini humo.

Taasisi hiyo ya kifedha ilitoa taarifa rasmi jana Jumamosi Novemba 22, 2025 ikisema kwamba taarifa ambazo zimekuwa zikisambaa sio za kweli na kuelezea kwamba zilikuwa zinahamasisha wateja wenye amana kwenye benki za biashara kuondoa fedha zao.

Wateja walishtuliwa kwamba mifumo ya benki itashambuliwa na wahalifu wa kimtandao na hivyo kusababisha kupotea kwa fedha zao na kutopatikana kwa huduma za benki.

“Benki Kuu inawahakikishia wananchi kuwa mifumo ya malipo ya Taifa pamoja na amana za wateja katika benki za biashara ni salama na inaendelea kuzisimamia kwa ufanisi na tija inayostahiki” ilisema taarifa hiyo rasmi.

BOT inashauri wananchi kuendelea kutunza amana zao katika benki kwani kuna manufaa mengi, yakiwemo kuongezeka kwa pesa kutokana na malipo ya riba au faida ya mwaka, fedha kutunzwa kwa usalama na uwepo wa bima ya amana endapo benki itafilisika.

Wanaosambaza taarifa hizo za kupotosha mitandaoni pia walionywa wakishauriwa waache mara moja, kwani tabia hiyo haina tija katika maendeleo ya sekta ya fedha, uchumi wa mtu mmoja mmoja au uchumi wa taifa kwa ujumla.

“Benki Kuu kwa kushirikiana na vyombo vya sheria, itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayeendelea kueneza taarifa hizi za upotoshaji” ilionya taasisi hiyo.

Share This Article