Mamlaka ya kudhibiti kawi nchini EPRA imetangaza bei za mafuta kama ilivyo ada kila tarehe 14 ya kila mwezi ambapo bei ya Super petrol imepanda huku ile ya dizeli na mafuta taa ikipungua.
Katika mabadiliko yaliyotangazwa jana Jumamosi Juni 14, 2025, EPRA ilifafanua kwamba bei ya Petroli imepanda kwa shilingi 2 na senti 69, bei ya dizeli imepungua kwa shilingi moja na senti 95 huku bei ya mafuta taa ikipungua kwa shilingi 2 na senti 06 kwa kila lita.
Kufuatia mabadiliko hayo, super petrol itauzwa shilingi 177.32, dizeli shilingi 162.91 na mafuta taa shilingi 146.93 kwa kila lita jijini Nairobi.
Kulingana na EPRA bei hizo zitatumika kuanzia leo Juni 15 hadi Julai 14 2025.
Taarifa ya EPRA ilielezea kwamba bei hizi mpya zinajumuisha ushuru wa thamani wa asilimia 16 kulingana na sheria ya fedha ya mwaka 2023, sheria iliyorekebishwa ya ushuru ya mwaka 2024 na mabadiliko ya viwango vya ushuru kulingana na mfumko wa bei.
Jijini Mombasa Petroli, dizeli na mafuta taa zitauzwa kwa shilingi 174.01, shilingi 159.62 na shilingi 143.64 mtawalia kwa kila lita bei ambazo zitakuwa shilingi 177.28, 163.23 na 147.30 jijini Kisumu.
Huko Nakuru petroli itauzwa shilingi 176.47, dizeli shilingi 162.41 na mafuta taa shilingi 146.47 kwa kila lita na huko Eldoret petroli, dizeli na mafuta taa vitauzwa shilingi 177.28, 163.24 na 147.30 mtawalia kwa kila lita.
EPRA ilielezea pia kwamba bei wastani ya super petrol iliyoagizwa kutoka nje iliongezeka kwa asilimia 0.35 kutoka shilingi elfu 76,166 kwa kila cubic metre mwezi Aprili mwaka 2025 hadi shilingi elfu 76,436 Mei 2025.
Dizeli ilipungua kwa kiwango cha asilimia 2.42 na mafuta taa kwa asilimia 5.14.