Mwanamuziki wa mtindo wa Dancehall kutoka Jamaica Moses Anthony Davis OD, maarufu kama Beenie Man amezungumzia uvumi uliosambazwa mitandaoni kumhusu.
Katika taarifa aliyochapisha kwenye akaunti yake rasmi ya Instagram, msanii huyo wa umri wa miaka 51 alikanusha madai ya kushambuliwa na kuibiwa.
“Kwa mashabiki, familia, marafiki, watu wenye nia njema na mapromota, nachukua fursa hii kuzungumzia uvumi ambao umekuwa ukisambazwa kunihusu.” alianza taarifa yake Beenie Man.
Msanii huyo aliendelea kwa kushukuru kwa mapenzi ambayo ameonyeshwa na mashabiki zake na kila mmoja aliyesimama naye kwa mema na mabaya, huku akiwahakikishia kwamba yuko salama na buheri wa afya.
“Ninaangazia muziki na familia na uvumi unaosambaa kwamba nimeibiwa na kupigwa risasi ni maneno ya uwongo na dhamira yake ni kusambaza woga na upuuzi.” alisema Beenie katika taarifa hiyo.
Alisema siku zote amekuwa akiamini katika uwezo wa muziki katika kuunganisha watu na wala sio kuwagawanya na akahimiza watu wainuane na kusaidiana.
Haya yanajiri wakati ambapo Beenie Man ambaye wengi humrejelea kama Daktari wa Dancehall ana mengi ya kusherehekea. Hivi maajuzi alishinda tuzo tatu katika tuzo za kimataifa za Reggae na muziki wa dunia mwaka 2025.
Alipokea tuzo za mtumbuizaji bora wa Caribbean, msanii bora wa matumizi na ujuzi wa jukwaa na tuzo ya kifahari ya mfalme wa muziki wa Dancehall.