Bebe Cool apeleka Break The Chains Tanzania

Amefika Tanzania baada ya kutangaza albamu hiyo yake ya kumi nchini kenya ambapo pia aliandaa hafla ya uzinduzi.

Marion Bosire
2 Min Read
Bebe Cool

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Uganda Bebe Cool yuko nchini Tanzania kwa ajili ya kutangaza albamu yake mpya iitwayo ‘Break The Chains’ kwenye vyombo vya habari.

Hii leo Cool pamoja na mke wake Zuena Kirema walikuwa katika studio za Bongo Five ambapo walizungumzia masuala kadhaa kuhusu muziki na hata ndoa yao.

Tanzania ndiyo nchi ya kwanza mwanamuziki huyo amezuru kwa ajili ya kutangaza kazi hiyo aliyozindua Mei 30, 2025 nchini Uganda na nchini Kenya mwanzo wa mwezi huu wa Julai.

Akiwa nchini Kenya alipata fursa ya kutangaza kazi hiyo ambayo ni albamu yake ya 10, kwenye vyombo mbali mbali vya habari akitaja Kenya kuwa kama nyumbani maanake ndiko alianzia muziki yapata miaka 30 iliyopita.

Msanii huyo alikutana na Kevin Wyre na Nazizi kwenye uzinduzi wa Kenya ikikumbukwa kwamba watatu hao waliwahi kufanya kazi pamoja kwenye kundi la muziki la East African Bashment Crew.

Akiwa kwenye mahojiano nchini Tanzania leo, Bebe Cool alionjeshwa nyimbo za mtindo wa singeli zikiwemo za Zuchu na wasanii wengine ambapo alifurahishwa na mtindo huo na kuahidi kufanya wimbo mmoja kwa mtindo huo.

Kuhusu Ndoa Cool alizungumzia kipindi ambapo mke wake alimwacha kwa muda wa mwaka mzima, jinsi aliteseka kiasi cha kumwimbia wimbo wa kumwomba arudi ndiposa akarudi.

Yeye na Zuena wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 25 sasa na wamebarikiwa na watoto 6.

Share This Article