Baraza la Sanaa la Taifa nchini Tanzania BASATA leo liliandaa kikao na mwanamuziki Ibraah katika afisi zake jijini Dar es Salaam.
Katika akaunti rasmi ya baraza hilo kwenye mtandao wa Instagram kulichapishwa picha ya pamoja ya katibu mtendaji wa BASATA Kedmon Mapana, Ibraah, meneja wake, mwanasheria wake na rais wa shirikisho la muziki nchini Tanzania.
Yaliyojadiliwa katika kikao hicho hayakuwekwa wazi lakini katika chapisho jingine, Ibraah alionekana akikabidhiwa kitabu cha mwongozo wa maadili katika kazi za Sanaa na katibu Mapana.
Awali BASATA ilikuwa imewaita Ibraah pamoja na mwanamuziki mwenza Harmonize baada yao kutupiana maneno ya kukoseana heshima mitandaoni.
Kabla ya hapo, Ibraah alikuwa ametumia Instagram kudai kwamba Harmonize amemwitisha shilinga Bilioni moja kabla ya kumruhusu kuondoka kwenye kampuni yake ya muziki ya kusimamia wasanii ya Konde Music.
Ibraah anaendeleza mchango mitandaoni akisema lengo lake ni kuchangisha pesa hizo alipe kampuni ya Konde Music ndiposa aweze kuondoka humo.
Kampuni hiyo ilitangaza pia kwamba msanii huyo amesimamishwa kushiriki kazi zozote za muziki na hata kufanya mahojiano ya vyombo vya habari au kuchapisha kwenye mitandao ya kijamiii masuala yanayohusiana na utata uliopo.
Harmonize alifafanua kwamba sio yeye binafsi amemwitisha Ibraah pesa hizo bali ni hitaji la mkataba ambao alitia saini.