Gavana wa kaunti ya Bomet Hillary Barchok na Gavana wa zamani wa kaunti ya Bungoma Wycliffe Wangamati wametakiwa kufika mbele ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC kuhusiana na tuhuma za ufisadi zinazowakabili.
Wawili hao ni miongoni mwa viongozi mashuhuri waliotakiwa kufika kwenye ofisi za tume hiyo Jumatatu ijayo asubuhi ili kuandikisha taarifa na kisha kufikishwa mahakamani ili kujibu mashtaka.
Kwenye taarifa jana Alhamisi, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Renson Ingonga aliagiza kushtakiwa kwa wawili hao kutokana na tuhuma za ufisadi.
Ingonga amethibitisha kupokea faili ya uchunguzi kutoka kwa EACC ikipendekeza kukamatwa kwa Gavana Barchok na Mkurugenzi wa kampuni ya Chemasus Construction Limited Evans Korir.
Mashtaka yanayowakabili ni pamoja na ulanguzi wa fedha, kujilimbikizia mali ya umma kwa njia ya ulaghai na mgongano wa maslahi miongoni mwa mengine.
Kwa upande wake, Wangamati pia anakabiliwa na mashtaka sawia ya mgongano wa maslahi miongoni mwa menngine.
Kwenye taarifa, Ingonga pia aliagiza uchunguzi zaidi kufanywa dhidi ya Magavana Kimani Wamatangi wa Kiambu na Mohammed Mahamud Ali wa Marsabit.
Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka ya mgongano wa maslahi miongoni mwa mashtaka mengine.
Katika kesi inayomkabili Gavana Mahamud, Ingonga alisema kuna mapungufu katika ushahidi ambayo yanahitaji kuangaziwa upya kwa uchunguzi zaidi.
Katika kaunti ya Kiambu, faili ya uchunguzi kutoka kwa EACC imependekeza kushtakiwa kwa Gavana Wamatangi pamoja na watu wengine saba kwa kwa mgongano wa maslahi na kujipatia mali ya umma kinyume cha sheria.
Hayo yanajiri wakati ambapo Rais William Ruto ameagiza kuwa wale wanaohusika katika visa vya ufisadi wachukuliwe hatua kali bila kujali hadhi yao katika jamii.