Baraza la Mawaziri laidhinisha taarifa ya sera ya bajeti ya 2025

Taarifa hiyo imeweka bajeti ya kiwango cha shilingi Trilioni 4.2 ya mwaka 2025/26

Marion Bosire
3 Min Read
Rais William Ruto,aongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri.

Rais William Ruto leo aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoidhinisha taarifa ya sera ya bajeti ya mwaka 2025 ambayo imeweka bajeti ya kiwango cha shilingi trilioni 4.2 ya mwaka 2025/26.

Matumizi hayo yanawakilisha asilimia 22.1 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na kujumuisha trilioni 3.09 za matumizi yanayojirudia, bilioni 725.1 za maendeleo na bilioni 436.7 mgao wa kaunti.

Mswada wa Ugavi wa Mapato wa mwaka 2025 unapendekeza mapato ya shilingi trilioni 2.8 yanayoweza kugawanywa ambapo shilingi bilioni 405.1 zimewekwa kando kwa ajili ya magatuzi.

Ufadhili wa ziada kutoka kwa serikali ya kitaifa na washirika wa kimaendeleo utafikisha mgao kwa kaunti kuwa shilingi bilioni 474.87.

Taarifa ya sera ya bajeti ya mwaka 2025 inaelezea maazimio ya serikali ya kustawisha maendeleo, kuhakikisha udhabiti wa kifedha na kuhimiza maendeleo ya mipango ya utunzaji mazingira.

Vipaumbele ni pamoja na kupunguza gharama ya maisha, kutokomeza njaa, kutengeneza fursa za ajira na kuvutia uwekezaji.

Serikali inalenga kuwa na ukuaji endelevu wa GDP wa kiwango cha asilimia 5.3 mwaka 2025 na 2026, pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika kilimo, huduma na ushirikiano kati ya sekta ya umma na ile ya kibinafsi.

Serikali inalenga pia kuondoa hatari ya deni la taifa kupitia kwa kulainisha matumizi, kuongeza vyanzo vya mapato na mabadiliko katika ushuru.

Usimamizi wa fedha za umma pia utaboreshwa ambapo haujatengewa ufadhili katika bajeti na kuwezeshwa kwa mfumo wa usajili na usimamizi wa mali ya umma wa IFMIS.

Baraza hilo la Mawaziri liliidhinisha pia bajeti ya pili ya ziada ya mwaka 2024/25, ambayo inatoa shilingi bilioni 344.8 zaidi kwa matumizi ambayo hujirudia na ya maendeleo. Idhinisho hili linafuatia mwingilio uliotokana na maandamano mwaka 2024.

Kikao hicho kiliidhinisha pia mipango ya kuboresha huduma kwa wasafiri katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), hatua itakayojumuisha kulainishwa kwa shughuli, kuboresha usalama na kuboresha miundombinu.

Mawaziri waliidhinisha pia mapatano kadhaa kuhusu kuwa nchi mwenyeji ili kuimarisha nafasi ya Kenya kama kitovu cha eneo hili cha mashirika ya kimataifa na kuidhinisha mapatano na Singapore kuhusu kuondoa utozaji ushuru mara mbili ili kuimarisha uhusiano wa biashara na uwekezaji ulimwenguni.

Share This Article