Baraza la Mawaziri laidhinisha Mswada wa Fedha wa mwaka 2025

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais William Ruto aongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri Aprili 29,2025.

Baraza la Mawaziri limeidhinisha Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2025, ambao unalenga kuziba mianya ya kodi badala ya kuanzisha kodi mpya.

Kulingana na taarifa ya Baraza la Mawaziri iliyotumwa kwa vyumba vya habari baada ya mkutano ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, Mswada huo unalenga kupunguza hatua za kuongeza ushuru.

Badala yake, Baraza la Mawaziri lilisema serikali inalenga kuimarisha mapato kupitia uongozi bora. Mabadiliko muhimu ni pamoja na kurahisisha urejeshaji wa kodi, kuimarisha sheria za mgongano wa  kodi, na kurekebisha sheria kuu za kodi ili kupunguza hali ya kukwepa kulipa ushuru.

Aidha, Baraza hilo la Mawaziri liliidhinisha ujenzi wa hospitali mbili za level IV katika kaunti za Bungoma na Kericho, kwa ushirikiano na benki ya maendeleo ya Afrika ili kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya.

Wakati huo huo, Majadiliano yanayohusu juhudi za kidiplomasia zinazoendelea na ujumbe wa kibalozi wa Kenya wa kutoa suluhu ya amani kwa  migogoro nchini Sudan pia yalitawala Mkutano huo.

Serikali ilisisitiza msimamo wa Kenya usioegemea upande wowote kuhusu suala hilo, na kuitaka Jamii ya kimataifa kuingilia kati kama wajibu wake chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kulinda maisha ya binadamu, mali na kuzuia matumizi ya silaha.

Kikao cha baraza la mawaziri kiliadhimisha kuhudhuria kwa mara ya  kwanza kwa Waziri wa Jinsia Hanna Cheptumo na mwenzake wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku.

Share This Article