Baraza la mawaziri limeidhinisha hatua ambazo zinalenga kuimarisha sekta ya utalii humu nchini ili kuboresha uwezo wake wa ushindani na kuhakikisha uendelevu.
Katika taarifa ya mkutano wa leo Jumanne wa baraza hilo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Rais William Ruto, ilikaririwa kwamba idadi ya watalii walioingia humu nchini mwaka 2024 iliongezeka.
Ongezeko hilo ni la kiwango cha asilimia 14.6 hadi watalii milioni 2.4, ambao walichangia mapato ya shilingi bilioni 452.2 kwa pato la taifa.
Huku watalii milioni tatu wakitarajiwa kuzuru Kenya mwaka huu wa 2025, serikali inapania kuangazia utalii endelevu, mikakati ya mauzo iliyoimarishwa na uwekezaji katika vifaa vya mikutano, vishawishi, makongamano na maonyesho.
Hatua nyingine ni pamija na kuwekeza katika miundombinu ya utalii wa usafiri wa baharini na maelezo mazuri katika utangazaji wa maeneo ya utalii.
Mipango muhimu katika kuimarisha utalii kulingana na baraza la mawaziri pia ni kukuza vitendo vya kutunza mazingira katika utalii, kupanua utalii wa kijamii na kulenga masoko muhimu kama Marekani na China.
Taarifa ya mkutano wa baraza la mawaziri inaelezea kwamba utalii wa usafiri wa baharini uliongezeka kwa kiwango cha asilimia 163.5%, na hivyo kukuza uwekezaji zaidi katika vifaa vya bandari.
Utalii wa ndani kwa ndani unaripotiwa pia kuimarika huku hoteli zikiripoti ongezeko la asilimia 12 la wageni waliokodisha vyumba vya kulala mwaka 2024.
Katika suala la utalii wa mikutano na makongamano, Rais alifahamisha baraza la mawaziri kwamba ujenzi wa kituo kikuu cha mikutano cha kimataifa cha Bomas utaanza katika muda wa wiki mbili zijazo.
Kiongozi wa taifa alisema hii ni hatua kubwa katika mpangp wa serikali wa kubadili eneo hilo kuwa la kiwango cha kimataifa.