Baraza jipya la Chuo Kikuu cha Nairobi lazinduliwa

Tom Mathinji
1 Min Read
Baraza jipya la Chuo Kikuu cha Nairobi lazinduliwa.

Waziri wa Elimu Julius Ogamba, amezindua rasmi Baraza jipya la Chuo Kikuu cha Nairobi, ambapo aliwataka wanachama wake kushirikiana, kuheshimu mipaka ya kitaasisi, na kujiepusha na udhibiti usiostahili wa usimamizi wa chuo hicho kikuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi ulioandaliwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, waziri Ogamba alisisitiza haja ya kushirikiana, kuheshimiana, na kuzingatia miundo ifaayo ya utawala.

Baraza hilo jipya litaongozwa na Profesa Chacha Nyaigoti Chacha.

Waziri huyo alitahadharisha dhidi ya kujirudia kwa changamoto zilizokumba baraza la awali, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, migogoro baina ya wadau, na jaribio la kuadhibu wafanyikazi nje ya mamlaka ya baraza hilo.

Alisema baraza lililovunjwa lilifeli katika kazi yake kutokana na ukosefu wa mashauriano, mwingilio wa majukumu ya wasimamizi, na kutotekeleza kazi yake ipasavyo, jambo ambalo liliathiri sio tu sifa ya chuo hicho, bali pia kutatiza harakati za ushirikiano muhimu.

Aidha alilamikia kesi nyingi za kisheria za chuo kikuu, ambazo zimekisiwa kuwa zaidi ya kesi 200 mahakamani, ambazo alisema zimefyonza rasilimali za umma na kubadilisha nia kuu ya kitaaluma ya taasisi hiyo.

TAGGED:
Share This Article