Barabara za mji wa Lungalunga zakarabatiwa

Martin Mwanje
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kwale Fatuma Achani amesema kuwa ataendeleza juhudi za kuboresha miundombinu ya manispaa ya Lungalunga katika mikakati ya kukuza biashara na uchumi katika eneo hilo lililopo katika mpaka wa Kenya na Tanzania.

Manispaa ya mji huo ulioko takriban kilomita 6 kutoka kwa mpaka wa Kenya na Tanzania, iliidhinishwa rasmi na Achani Julai 11, 2022, ikiwa kivutio kikubwa cha biashara kati ya wakazi wa mji huo na wenyeji wa nchi jirani ya Tanzania.

Hiyo ilifikisha nne idadi ya manispaa katika eneo hilo ikiwemo Kwale, Diani, Kinango na Lungalunga.

Akizungumza alipokuwa akizindua ukarabati wa barabara ya Ziwani kuelekea kwenye soko la Lungalunga, Gavana huyo aliwahimiza wakazi kushirikiana na serikali yake   katika juhudi za kuupandisha hadhi mji huo, akisema kuboreshwa kwa mji huo kutasaidia kukuza uchumi wa kaunti kupitia biashara.

Kiongozi huyo aidha ameahidi kutafuta suluhu ya kudumu kutokana na suala tata la ukosefu wa maji katika mji huo, akisema kwa muda mrefu, suala hilo limekuwa likitatiza shughli mbalimbali zinazoendelea kwenye mji huo.

Share This Article