Barabara mpya yaleta tabasamu kwa wakazi wa Kinangop Kaskazini

Tom Mathinji
2 Min Read
Ujenzi wa barabara kaunti ya Nyandarua.

Wakazi wa Kinangop Kaskazini, wana sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kitaifa kutimiza ahadi yake ya kukamilisha ujenzi wa barabara iliyokwama katika Kaunti ya Nyandarua.

Wakizungumza katika kijiji cha Karai, Kinangop Kaskazini, wakazi hao walielezea matumaini mapya ya maendeleo, baada ya ujenzi wa barabara ya lami ya Captain-Wanjohi-Ndunyu Njeru kuanza rasmi katika eneo hilo.

Kinangop Kaskazini ni maarufu kwa kwa kilimo cha maua na mboga, huku wakulima wakisema hawatahesabu hasara ya mazao yao kuharibika kutokana na miundombinu mibovu.

Barabara hiyo inayojengwa sasa inaunganisha vijiji muhimu kama vile Kwa Mbekenya, Karima Karai na Kiambariki—eneo linalojivunia uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na ufugaji wa maziwa.

Ujenzi wa barabara kaunti ya Nyandarua.

Mmoja wa wakazi Ruth Njoki, alisimulia jinsi kwa muda mrefu amekuwa akiwasaidia wanawake kujifungua kando ya barabara kutokana na hali mbaya ya barabara. Kwa sasa, anasema swala hilo litazikwa katika kaburi la sahau.

Kulingana na wakazi wa eneo hilo, kwa muda wa miaka mingi, wamekuwa wakikejeliwa kutokana na hali mbovu ya barabara.

Walimpongeza Rais William Ruto kwa kutimiza ahadi kufuatia safari yake ya hivi maajuzi katika kaunti ya Nyandarua, pamoja na mbunge wao Kwenya Thuku, kwa juhudi zake za kupigiwa mfano katika kushawishi Serikali ya Kitaifa kukamilisha miradi iliyokwama.

Share This Article