Mwanamuziki Bahati na mke wake Diana wamezindua kampuni yao ya kamari kwa jina Bahati Bet.
Kampuni hiyo ilizinduliwa kwenye hafla ambayo walikuwa wameipa jina la “The Bahatis’ Big day” ambayo wengi walitarajia iwe harusi.
Hafla hiyo ilikuja mwisho wa zawadi 8 ambazo amekuwa akimpa Diana kama njia ya kusherehekea miaka minane ya kuwa pamoja.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bahati alisema kwamba anaombea kila mmoja aweze kufungua biashara ambayo amekuwa akipanga kufungua.
Mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya EMB Records alisema pia kwamba amekuwa akitangazia wengine kampuni zao za kamari lakini sasa hii ni yake, huku akimtangaza Diana kuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo.
Diana alitoa hotuba yake kama mkurugenzi mkuu akisema kwamba wamekuwa wakijituma kwa muda wa miezi kadhaa kuunda kampuni hiyo ya kamari na sasa wamefanikiwa.
Wawili hao walitangaza pia siku yao ya harusi ambayo ni tarehe 28 mwezi Oktoba mwaka huu wa 2025, tarehe hiyo inawiana na tarehe ambayo uhusiano wao ulianza rasmi miaka minane iliyopita.
Bahati alimchumbia Diana kwa mara ya pili siku chache zilizopita hatua iliyomfanya Diana abubujikwe na machozi ya furaha.
Baada ya kuvishwa pete kwa mara ya pili, Diama alisema anatamani kufanya harusi kubwa ambayo ataalika wageni wengi kadri ya uwezo wake.