Kemi Badenoch ameahidi kuleta mabadiliko katika chama cha Conservative cha Uingereza baada ya kuibuka mshindi wa kinyang’anyiro cha uongozi wa chama hicho.
Ameahidi kurejesha wapiga kura waliokuwa wafuasi wa chama hicho ambao wamekiasi anapokuwa mwanamke wa kwanza mweusi ambaye amewahi kuongoza chama hicho.
Badenoch alimshinda Robert Jenrick wa umri wa miaka 42 kwa kura 12,418 katika kinyang’anyiro cha kujaza nafasi ya Rishi Sunak, aliyeongoza chama hicho kupata ushinde wa kihistoria kwenye uchaguzi wa mwezi Julai.
Kwenye hotuba yake ya ushindi, Kemi aliahidi kukifanya upya chama cha Conservative.
Kiongozi huyo wa sita wa chama cha Conservatibe katika muda wa chini ya miaka tisa ana kibarua kigumu cha kuunganisha tena wanachama wa chama hicho na kuongoza upinzani kwa serikali ya sasa.
Kulingana naye wakati umewadia wa kuwa wakweli na kukubali kwamba makosa yalitendeka na sasa yanafaa kurekebishwa.
Badenoch ambaye aliamua kutoweka wazi mikakati yake ya kubadilisha chama cha Conservative wakati wa kampeni, aliamua kuangazia kurejeshea chama hicho kanuni zake za mwanzo.
Sasa wadadisi wanasubiri kuona atakaowachagua kujiunga na uongozi wa chama anapolenga kuleta mabadiliko.
Badenoch alichaguliwa mbunge mwaka 2017 baada ya kufanya kazi katika sekta ya benki na ile ya teknolojia ya mawasiliano na ameahidi kuwapa fursa za kazi wanachama wa chama hicho waliowania nyadhifa mwezi Julai.