Baba Levo amjibu Mwijaku

Mwijaku alidai kwamba Diamond ameumizwa na ndoa ya mpenzi wake wa awali Hamisa Mobeto.

Marion Bosire
2 Min Read

Mtangazaji wa Wasafi Fm inayomilikiwa na mwanamuziki Diamond Platnumz Baba Levo, amemjibu mtangazaji Mwijaku kutokana na kauli yake kuhusu Diamond baada ya Hamisa Mobeto kuolewa.

Mwijaku aliyehusika pakubwa kwenye harusi ya Hamisa Mobeto alisikika akiambia wanahabari kwamba Diamond anapapatika kwa kuona mpenzi wake wa zamani ameolewa.

Alipoulizwa kauli yake kuhusu madai ya Mwijaku, Baba Levo kwanza alishangaa Mwijaku ni nani ambaye akisema jambo ni lazima yeye aulizwe atoe kauli.

“Kwani huyu Mwijaku ni nani? Mwijaku ni nani kwamba akisema jambo lazima nije niulizwe mimi?” alishangaa Baba Levo.

Baadaye aliendelea kusema kwamba Diamond Platnumz ana mpango wa kumwoa mwanamuziki mwenza Zuchu na watasherehekea kwa siku 17 mfululizo katika sehemu mbali mbali za Tanzania.

Alisema pia kwamba tofauti na harusi nyingine ambapo watu wanachinja mbuzi, kwenye harusi ya Diamond kutachinjwa ngamia 21 ili wageni wale washibe.

Baba Levo, bila kutaja yeyote, alisema kwamba, “watu hawaoani kwa kukurupuka, hawaoani kwa kuiga, watu wanaoana kwa sababu ya mapenzi na kwa mipango iliyopangwa.”

Mtangazaji huyo alipuuzilia mbali madai kwamba harusi ya Hamisa Mobeto ilifanana na ya Davido mwanamuziki wa Nigeria.

Diamond Platnumz aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Hamisa Mobeto, baada ya Hamisa kuigiza kwenye video ya wimbo “Salome” wa miaka minane iliyopita.

Wana mtoto mmoja wa kiume kwa jina Dylan.

Share This Article