Mafarakano yamechacha katika muungano wa Azimio kufuatia madai kwamba kiongozi wa muungano huo Raila Odinga ameridhia kuunda serikali ya kitaifa na Rais William Ruto.
Baadhi ya wanachama wa ODM na wandani wa Raila wanasemekama kuwa mbioni kutajwa kwenye nusu iliyosalia ya Baraza Jipya la Mawaziri itakayotangazwa na Rais Ruto.
Yamkini mafarakano hayo ndio sababu iliyomsababisha Rais Ruto kutotaja Baraza kamili la Mawaziri leo Ijumaa.
“Mashauriano zaidi yanaendelea na baadaye nitataja majina zaidi kadiri muda unavyosonga mbele,” alisema Rais Ruto wakati akihutubia taifa kutoka Ikulu ya Nairobi.
Awali, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alitangaza kuwa vyama tanzu vya Azimio havitakubali kujiunga na serikali ya Rais Ruto.
Alisema kufanya hivyo itakuwa ni kuwasaliti vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakiandamana kushinikiza kutekelezwa kwa mabadiliko nchini.
Vyama hivyo ni Wiper, kile cha mrengo wa Jubilee unaoongozwa na mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni, DAP-K cha Eugene Wamalwa, Narc K cha Martha Karua na PNU.
“Hatutashiriki au kuunga mkono serikali ya kitaifa ya wigo mpana iliyopendekezwa ikiongozwa na Kenya kwanza,” alisema Kalonzo.
“Ikiwa mwachama wetu yoyote ataamua kujiunga na serikali ya kitaifa ya wigo mpana iliyopendekezwa ikiongozwa na Kenya kwanza, hatutakuwa sehemu ya uamuzi huo,” aliongeza Kalonzo aliyeandamana na Wamalwa na Kioni miongoni mwa viongozi wengine wa Azimio.
Chama cha ODM hakikushiriki mkutano huo, ishara kwamba ni chama hicho kilichozungumziwa.
Baadhi ya viongozi wa chama cha ODM wamenukuliwa wakisema wako tayari kutalikiana na Azimio ikiwa hatua ya kujiunga na serikali italazimu hilo kufanyika.