Azawi atia saini mkataba mpya na Swangz Avenue

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki wa kike nchini Uganda Azawi ambaye amewahi kushinda tuzo kadhaa ametia saini mkataba mpya wa albamu nyingi na Swangz Avenue.

Azawi ambaye hina lake halisi ni Priscilla Zawedde alijiunga na Swangz Avenue mwaka 2019, na amejizolea umaarufu katika tasnia ya muziki ya Uganda kwa kipindi cha miaka mitano.

Umahiri wake katika uandishi wa nyimbo, sauti yake ya kipekee na ubunifu wa kisanii ndivyo baadhi ya vitu vinavyofanikisha kazi yake.

Safari yake na Swangz Avenue imetoa mafanikio kadhaa makubwa ambapo alitoa mkusanyiko wake wa kwanza wa nyimbo yaani EP iitwayo ‘Lo Fit’ ya mwaka 2020.

Mwaka 2021 alitoa albamu iliyosifiwa sana ya ‘African Music’, inayochukuliwa kuwa moja ya albamu zenye athari kubwa zaidi Uganda katika miaka ya hivi karibuni.

Kando na kazi hizo Azawi ameweza kuweka alama yake kwenye majukwaa makubwa kimataifa na hata nyumbani kama vile tamasha la kusisimua la Azawi African Music katika uwanja wa Lugogo mwaka 2022.

Zaidi ya muziki, Azawi amejiimarisha kama mshiriki muhimu wa tamaduni na mshirika wa chapa mbalimbali. Uhalisia wake na ushawishi wake wa kitamaduni vimemletea mikataba mikubwa ya uwakilishi na chapa kubwa kubwa.

Kuhusu mkataba huu mpya Azawi alieleza furaha yake kwa hatua inayofuata, akiongeza kwamba Swangz Avenue imekuwa nyumbani tangu mwanzo.

“Mkataba huu mpya ni ukumbusho kwamba bado tuna mengi ya kuunda, kuboresha na kushiriki na dunia. Ninaingia katika sura mpya ya nafsi yangu kimuziki, kiubunifu na kibinafsi” alisema msanii huyo.

Alishukuru usimamizi wake unaomjumuisha Julius Kyazze, mwanzilishi mwenza na mkurugenzi mtendaji wa Swangz Avenue.

Kyazze alithibitisha upya dhamira ya lebo kwa safari ya Azawi ambaye alisema anawakilisha kila kitu ambacho kampuni hiyo inasimamia kama uhalisia, ubora, na ubunifu.

“Tangu siku ya kwanza, tulijua ana kitu cha kipekee sana. Mkataba huu mpya wa albamu nyingi ni dhamira ya kumuinua hadi kilele cha kimataifa zaidi.” Alimalizia Kyazze.

Share This Article