Serikali ya Australia imetangaza kuwa itaitambua rasmi Palestina kama taifa huru katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika mwezi Septemba, hatua inayofuatia maamuzi sawa yaliyofikiwa na mataifa kama Uingereza, Ufaransa na Kanada.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.
Kwa mujibu wa Albanese, uamuzi huo umetanguliwa na makubaliano muhimu kati ya Australia na Mamlaka ya Palestina, yakiwemo masharti ya kupokonywa silaha kwa makundi yenye silaha, kufanyika kwa uchaguzi mkuu, na uthibitisho wa Palestina kulitambua taifa la Israel na haki yake ya kuendelea kuwepo.
“Suluhishila kutambua kuwa ni mataifa mawili tofauti ndilo tumaini la kweli kwa binadamu kuvunja mzunguko wa vurugu katika Mashariki ya Kati, na kumaliza migogoro, mateso na baa la njaa linaloikumba Gaza,” alisema Waziri Mkuu huyo siku ya Jumatatu.
Hata hivyo, Israel ambayo inaendelea kukabiliwa na shinikizo la kimataifa kusitisha vita vinavyoendelea Gaza imekosoa hatua hiyo, ikisema kuwa kutambuliwa kwa taifa la Palestina ni sawa na “kutunuku ugaidi”.
Tangu Jumamosi iliyopita, watu watano wamefariki dunia kutokana na njaa na utapiamlo huko Gaza, na kufikisha idadi ya vifo kutokana na hali hiyo kuwa 217, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas.
Aidha, tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel mwaka 2023, zaidi ya watu 61,000 wamepoteza maisha, kwa mujibu wa idadi iliyotolewa na mamlaka hiyo.
Mashambulizi hayo ya Israel yalizuka kufuatia uvamizi mkubwa ulioongozwa na kundi la Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba mwaka huo, ambapo watu wapatao 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Palestina ambayo inasimamia baadhi ya maeneo ya Ukingo wa Magharibi yanayokaliwa na Israel imesema kutambuliwa kwa taifa hilo ni ishara ya kuongezeka kwa uungwaji mkono wa kimataifa kwa haki ya Wapalestina ya kujitawala.
Waziri Mkuu Albanese alieleza kuwa uamuzi wa serikali yake umetokana na ahadi ya Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, kuwa Hamas haitakuwa na nafasi yoyote katika uongozi wa taifa la Palestina litakapoundwa.
Hatua hii pia inatajwa kuwa zao la mashauriano ya karibu kati ya Australia na viongozi wa mataifa mengine, yakiwemo Uingereza, Ufaransa, New Zealand na Japan, yaliyofanyika katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
“Tunaamini kuwa huu ni wakati wa fursa ya kihistoria, na Australia iko tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kuitumia ipasavyo,” alisema Albanese katika mkutano na waandishi wa habari.
Jumapili iliyopita, maelfu ya waandamanaji waliounga mkono taifa la Palestina walishiriki maandamano makubwa yaliyovuka Daraja la Bandari la Sydney, siku moja baada ya mahakama kuidhinisha maandamano hayo kufanyika.