Aunty Ezekiel ashauri mabinti wavae kimaadili

Ushauri wake unafuatia kikao cha ukosoaji na bodi ya filamu nchini Tanzania kutokana na picha aliyochapisha mitandaoni.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa filamu za Bongo nchini Tanzania Gwantwa Ezekiel Grayson, maarufu kama Aunty Ezekiel ameshauri mabinti wa Tanzania wawe wakivaa mavazi yanayodumisha maadili ya jamii.

Ushauri wake ulijiri baada ya kikao na bodi ya filamu nchini Tanzania iliyokuwa imemwalika kwa kikao cha ukosoaji kufuatia picha aliyochapisha mitandaoni.

Msanii huyo ambaye pia ni mfanyabiashara, alichapisha picha iliyoonyesha sehemu kubwa ya mwili wake kwenye Instagram akitangaza bidhaa zake za kutunza ngozi, picha ambayo ilisababisha akosolewe na wengi.

Kufuatia hilo, bodi ya filamu ilimwalika kwa kikao leo bila kutaja sababu za kikao hicho lakini tayari wengi walikuwa wamekisia.

Ezekiel anasema katika kikao cha leo, alipatiwa ushauri kuhusu jinsi anaweza kuendeleza biashara yake huku akitunza sifa yake kama msanii ambaye mara nyingi huchukuliwa kuwa kioo cha jamii.

Katika mahojiano na wanahabari baada ya kikao hicho, Aunty Ezekiel alifichua kwamba mume wake ambaye ni mwanamuziki kusah alikuwa mtu wa kwanza kumkosoa alipochapisha picha hiyo na akamwelekeza aifute na anasema aliifuta mara moja.

Share This Article