Askofu mstaafu wa kanisa katoliki Philip Anyolo Sulumeti amefariki. Tangazo la kifo chake lilitolewa na Askofu Joseph Obanyi wa dayosisi ya Kakamega ya kanisa katoliki.
Kulingana na Obanyi, Askofu Sulumeti aliaga dunia jana Novemba 9, 2025 saa tano usiku akiendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Nairobi.
Askofu huyo wa Kakamega alihimiza waumini waendelee kumwombea mwendazake huku mipango ya mazishi ikianzishwa.
“Kwa watu wote wa Mungu wa Kakamega, jamaa na marafiki, tunawapa pole na kuahidi kuendelea kuwaombea kipindi hiki kigumu” alisema Askofu Obanyi.
Askofu Sulumeti alizaliwa Agosti 15, 1937 katika kijiji cha Kobur, wilaya ya Busia, dayosisi ya Bungoma ya kanisa katoliki.
Alisoma shule ya msingi ya nyumbani kabla ya kuendelea na masomo yake katika shule kadhaa za upadri katika eneo la Afrika mashariki.
Baadaye alielekea Roma, Italia kwa masomo zaidi ambapo alifuzu kutoka taasisi ya St. Peter’s Pontifical baada ya kukamilisha masomo kuhusu dini na sheria za dini.
Agosti 20, 1972 ndio alitawazwa na miaka minne baadaye akafanywa Askofu wa dayosisi ya Kisumu ambapo alichukua mahala pa Askofu Joannes de Reeper.
Februari 28, 1978 Askofu Sulumeti alichaguliwa askofu wa kwanza wa dayosisi ya Kakamega, jukumu alilokumbatia kwa kujitolea.
Uongozi wake ulijiri wakati ambapo eneo hilo lilikuwa limekumbwa na changamoto kadhaa za kijamii na kiuchumi na akapata kujulikana haraka kutokana na upole wake na uongozi katika maendeleo ya kijamii.
Sulumeti aliongoza ukuaji wa shule zilizokuwa zikiendeshwa na kanisa katoliki akiamini kwamba elimu ndiyo msingi wa mabadiliko katika jamii.
Alistaafu Disemba 5, 2014.