Arsenal ,Chelsea watamba,Man U wapigwa kabari nyumbani

The Gunners wameititiga Ipswich Town mabao 4-0 ugani Emirates, Leandro Trossard akifunga mawili, moja katika kila kipindi, huku Gabriel Martinelli na Ethan Nwaneri wakiongeza moja kila mmoja.

Dismas Otuke
1 Min Read

Arsenal na Chelsea wamesajili ushindi huku Manchester United wakibumbuazwa nyumbani na Wolves, katika mechi za raundi ya 33 za ligi kuu Uingereza EPL zilizosakatwa Jumapili jioni.

The Gunners wameititiga Ipswich Town mabao 4-0 ugani Emirates, Leandro Trossard akifunga mawili, moja katika kila kipindi, huku Gabriel Martinelli na Ethan Nwaneri wakiongeza moja kila mmoja.

Chelsea, wakiwa ugenini Craven Cottage, walikuwa na wakati mgumu, kabla ya kutoka nyuma na kulazimisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Fulham.

Alex Iwobi aliwaweka wenyeji uongozini katika dakika ya 20 na kudumu hadi mapumzikoni.

Tyrique George alisawazisha bao hilo kwa wageni The Blues dakika saba kabla ya kipenga cha mwisho, huku Pedro Neto, akifunga la ushindi dakika ya 93.

Hata hivyo, Mashetani Wekundu, Manchester United, waliendelea kuyumbayumba baada ya kupigwa bao moja bila jawabu ugani Old Trafford na Wolves.

Mhispania Pablo Sarabia alipachika kimiani goli pekee na la ushindi kwa wageni Wolves dakika ya 77.

Share This Article