Angela Okorie akanusha madai ya kukamatwa na polisi

Mwigizaji huyo alitoweka mitandaoni kwa muda na inaaminika alikuwa amezuiliwa na polisi.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji maarufu wa Nigeria Angela Okorie anayefahamika pia kama Legit Queen amekanusha madai ya kukamatwa na maafisa wa polisi.

Okorie alirejea kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutokuwepo kwa muda huku minong’ono ikisheheni kwamba wakati alikuwa hayuko mitandaoni, alikuwa amezuiliwa na polisi.

Inadaiwa kwamba polisi walighadhabishwa na video aliyochapisha mwigizaji huyo, ambaye alifanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio , inayomwonyesha akikimbia huku akipatiwa ulinzi na maafisa wa polisi.

Uvumi mwingine ulidai kwamba alikamatwa kutokana na malalamishi yaliyowasilishwa kwa maafisa wa usalama na Mercy Johnson Okojie ambaye pia ni mwigizaji.

Awali mwandaaji filamu wa Nollywood Stanley Ontop alikuwa amesema kwamba mume wa Regina Daniels aitwaye Ned Nwoko na Mercy Johnson walikuwa wamewasilisha malalamishi dhidi ya Angela Okorie.

Angela alisikika akidai kwamba Mercy Johnson anaugua ilipobainika kwamba alikuwa amepoteza uzani wa mwili kwa kiwango kikubwa, usemi uliomkasirisha Regina Daniels ambaye ni rafiki wa karibu wa Mercy Johnson.

Daniels alimjibu Okorie kwa maneno makali naye Okorie akamshambulia kwa kuolewa na mzee aliyemzidi umri aliyemrejelea kama babu.

Inadaiwa kwamba Ned na Mercy walitaka kutumia ushawishi wao kusababisha Angela Okorie afungwe kwa miaka 18 kwa kuwachafulia sifa mitandaoni.

Okorie hata hivyo anasema kwamba alialikwa na polisi na akaitikia wito wao wala hakukamatwa inavyodaiwa. Alisema pia kwamba hatakuwa anajibu uvumi wowote kumhusu mitandaoni.

Share This Article