Spika wa zamani wa Bunge la Tanzania Job Yustino Ndugai ameaga dunia. Hayo yametangazwa na Spika wa Bunge hilo Dkt Tulia Ackson.
Kulingana na Ackson, kifo cha Ndugai kimetokea leo Jumatano jijini Dodoma, huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijaelezwa.
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma. Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema Tulia.
Spika mstaafu Ndugai kabla ya kifo chake aliibuka mshindi katika kura za maoni, kuwania ubunge katika jimbo la Kongwa mkoani Dodoma katikati mwa Tanzania, zilizopigwa hivi karibuni.
Ndugai alihudumu katika nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania kwa miaka 6, kuanzia mwishoni mwa 2015 hadi alipojiuzulu Januari, 2022.
Kabla ya hapo alihudumu kama Naibu Spika kati ya Novemba, 2010 Na Novemba, 2015.
Pamoja na kuwa mahiri kwa kuzifahamu vema kanuni za Bunge, aliwahi kukosolewa kwa kutoa kauli tata ikiwemo kusema alikuwa na uwezo wa kumzuia mbunge yeyote asizungumze kabisa bungeni.
Pia aliwahi kukosolewa kwa kusema aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli angelazimishwa kuendelea kugombea urais baada ya kumalizika vipindi viwili vinavyoruhusiwa kikatiba ”atake asitake”.