Alexis Dusabe mwimbaji wa nyimbo za injili wa asili ya Rwanda aliadhimisha miaka 25 ya uimbaji katika hafla ya kufana Septemba 14, 2025.
Dusabe mmoja wa waanzilishi wa sekta ya nyimbo za injili nchini Rwanda alialika wadau wa sekta ya muziki kwa sherehe hiyo katika hoteli ya Dove iliyoko Gisozi, jijini Kigali nchini Rwanda.
Mwimbaji huyo anataja safari yake ya muziki kuwa yenye changamoto nyingi lakini anafahamu ndiyo njia ya yeyote ambaye anaamua kujaribu.
Dusabe alitumia hafla hiyo pia kufichua albamu yake ijayo kwa jina “Amavuta y’Igiciro” ambapo waliohudhuria walipata fursa ya kusikiliza nyimbo zilizoko zitakazozinduliwa rasmi Disemba 14 katika tamasha.
Kulingana naye, albamu hiyo ilizaliwa kutokana na hadithi ya mwanamke aliyepatikana akishiriki uzinzi, akisisitiza kuhusu upendo na neema ya Mungu.
Waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Israel Mbonyi, Mariya Yohana, Masamba Intore, Butera Knowless, Nel Ngabo, Bosco Nshuti, mwandaaji wa muziki Clement Ishimwe, wachekeshaji na hata waigizaji wa filamu.