Mwanamuziki na mfanyabiashara Esther Akoth Kokeyo maarufu kama Akothee amefichua uhusiano uliopo kati ya babake Mzee Jose Kokeyo na marehemu Raila Amolo Odinga.
Maelezo yake yanafuatia video aliyochapisha awali inayomwonyesha akizungumza na babake mzazi kwa njia ya simu kutoka ughaibuni asijue kwamba mzee tayari alikuwa anafahamu kuhusu kifo cha Raila.
Mzee Kokeyo anasikika akilia kwenye mawasiliano hayo ingawa haonekani na Akothee anaelezea kwamba kifo cha Raila kimewagusa sana kama familia.
Kulingana na Akothee, babake alikuwa yatima ambaye alipata usaidizi kutoka kwa familia ya Odinga kiasi kwamba alipelekwa ng’ambo kwa ajili ya masomo hususan nchini Urusi, wakati huo Raila akisoma Ujerumani.
Akothee alifichua pia kwamba babake alikuwa mwanamuziki aliyefahamika zaidi kwa nyimbo kama ‘Safari Ya Tanganyika’ na’Oginga Ajuma’ kati ya nyingine.
Mwanamuziki huyo anasema babake alipofika Urusi mtindo wake wa muziki ulibadilika kiasi kutokana na athari ya muziki wa huko.
Sasa mwimbaji huyo anaomba mashabiki zake wamtunzie wazazi wake iwapo watawaona kwenye mazishi ya Raila hapo kesho nyumbani kwake huko Bondo kaunti ya Siaya.
Raila aliaga dunia asubuhi ya Oktoba 15, 2025 kutokana na mshtuko wa moyo ambao kulingana na binti yake Winnie ulisababishwa na mazoezi yake ya matembezi.