Sasa ni rasmi kwamba Agosti 27 kila mwaka itakuwa ikiadhimishwa kama Siku ya Katiba.
Ni siku hiyo ambapo katiba ya sasa iliidhinishwa wakati wa utawala wa Hayati Mwai Kibaki mnamo mwaka 2010.
Hata hivyo, kinyume cha matarajio ya wengi, Agosti 27 haitakuwa sikukuu ambayo Wakenya wanaweza wakapata fursa ya kupumzika.
Badala yake, Rais William Ruto ametangaza kuwa siku hiyo itakuwa ikiadhimishwa kila mwaka kwa kusudi la kuwakumbusha Wakenya wajibu wao wa kuheshimu, kulinda na kutekeleza Katiba.
“Siku ya Katiba itaadhimishwa kote nchini Kenya na kwenye balozi zetu zote ughaibuni kama siku iliyotengwa kuhuisha dhamira yetu ya pamoja kwa maadili ya katiba kwa kuhamasisha mazungumzo ya kitaifa juu ya utekelezaji katiba, uongozi, na utawala wa sheria,” alisema Rais Ruto kwenye tangazo lake leo Jumatatu.
“Ingawa Siku ya Katiba itasalia kuwa siku ya kazi, asasi zote za serikali katika mihimili yote ya serikali na ngazi zote mbili za uongozi, zikiwemo shule, zitaratibu, kuandaa, na kushiriki shughuli za raia siku hiyo ili kukuza uelewa wa katiba na ushiriki wa raia.”