Rais William Ruto amesema kuna haja ya kuwekeza katika watu, afya yao pamoja na elimu ili kuhakikisha ukuaji jumuishi na ustawi wa pamoja barani Afrika.
Amesema licha ya chumi za Afrika kukua kwa kasi kiuchumi, hazijafanikiwa mno katika kuungamiza umaskini miongoni mwa raia wake.
“Chumi za Afrika ni miongoni mwa zile zinazokua kwa kasi zaidi duniani, huku Pato Ghafi la Taifa, GDP ya eneo la Sub-Saharan ikikadiriwa kukua kwa asilimia 4 ikilinganishwa na wastani wa dunia wa asilimia 3. Hata hivyo, ukuaji huu haujaangazia vya kutosha suala la kuangamiza umaskini, kubuni nafasi za ajira au hata huduma za afya na elimu,” alisema Ruto wakati akitoa hotuba kuu kwenye kikao juu ya Nguzo ya Jamii kilichofanyika wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, TICAD uliomalizika leo Ijumaa mjini Yokohama nchini Japani.

“Isitoshe, ili ukuaji jumuishi na ustawi wa pamoja utimie kwa ajili ya raia wetu na kutomwacha yeyote nyuma, lazima tuwekeze kwa kiwango kikubwa katika watu, afya yao, elimu na hasa hali yao njema,” aliongeza Ruto aliyehudhuria mkutano huo pamoja na makumi ya viongozi wengine kutoka barani Afrika.

Mkutano wa TICAD ulimalizika kwa kuidhinishwa kwa Azimio la Yokohama linaloangazia ushirikiano unaolenga uendelezaji wa rasilimali watu na usambazaji thabiti wa rasilimali za madini kati ya Japani na bara la Afrika.