Afisi ya kushughulikia pasipoti kufunguliwa Malindi

Tom Mathinji
1 Min Read
Serikali kufungua afisi ya kushughulikia Pasipoti Malindi.

Serikali itafungua afisi ya kushughulikia pasipoti mjini Malindi, kaunti ya Kilifi, ili kuhakikisha wakazi wa eneo hilo wanapata hati hiyo muhimu wanapotafuta ajira ughaibuni.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Gede wakati wa sherehe za Mashujaa, Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Malindi David Lusava, alisema hatua hiyo itasitisha mahangaiko ya wakazi wa eneo hilo ambao hulazimika kusafiri hadi Mombasa na Nairobi kutafuta stakabadhi hiyo.

“Hivi karibuni kupitia wizara ya Usalama wa Taifa, tutafungua afisi ya kushughulikia pasipoti Malindi. Kuanzia mwaka ujao, wale wote wanahitaji paspoti hawatasafiri kuelekea Mombasa au Nairobi, pasipoti zitapatikana hapa,” alisema Lusava.

Mtawala huyo alidokeza kuwa vijana wengi katika eneo hilo wanaotafuta ajira ughaibuni, hukumbwa na changamoto za kupata hati hiyo ya kusafiri, akihakikisha kuwa changamoto hiyo sasa itazikwa katika kaburi la sahau.

Share This Article