Afisa wa polisi Kibera akamatwa kwa madai ya kuitisha rushwa

Martin Mwanje
1 Min Read
Konstebo wa Polisi Philip Ochieng Adongo

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imemkamata Konstebo wa Polisi Philip Ochieng Adongo aanayehudumu katika kituo cha polisi cha Sarangombe kwa madai ya kuitisha na kupokea hongo kuhusiana na kesi ya ubakaji.

Inadaiwa kuwa Adongo aliitisha hongo ya shilingi 4,000 kutoka kwa mlalamikaji ili kumkamata mshukiwa wa ubakaji wa binti ya mlalamikaji huyo.

Madai ya ubakaji huo yalikuwa awali yameripotiwa kwenye kituo hicho cha polisi kupitia kitabu cha matukio ambayo nambari yake ni OB No. 16/18/07/2025.

Agosti 13, EACC ilifanya operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa Adongo na raia mmoja aliyetambuliwa kama George Otieno Oywer.

Oywer anatuhumiwa kupokea hongo kwa niaba ya afisa huyo.

Wawili hao walifikishwa katika makao makuu ya EACC kuandikisha taarifa wakati wakisubiri kufikishwa mahakamani.

TAGGED:
Share This Article