Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini, EACC imemkamata afisa wa Halmashauri ya Bandari Nchini, KPA kutokana na mgongano wa maslahi na udanganyifu katika utoaji wa zabuni.
Janet Mwendwa sasa atakabiliwa na mashtaka ya kupatiana kwa ulaghai zabuni yenye thamani ya shilingi milioni 6.4 kwa kampuni inayomilikiwa na bintinye.
EACC inasema Janet ambaye anashukiwa kufanya biashara na KPA kupitia kampuni ya bintiye, alishiriki mchakato wa kutathmini zabuni hiyo ambayo baadaye ilikabidhiwa bintiye.
Mshukiwa alipelekwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi ya Mombasa ili kukiri mashtaka.
Janet alikamatwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kukubaliana na mapendekezo ya EACC kuwa afunguliwe mashtaka ya mgongano wa maslahi, upataji wa mali ya umma kinyume cha sheria, ulaghai katika utoaji zabuni na upatianaji wa nyaraka zisizokuwa za kweli kinyume cha sheria.