Naibu Afisa wa Ukusanyaji Mapato katika Kampuni ya Huduma za Maji na Maji Taka ya Nairobi (NWSC) Teresia Chepkemoi Chepkwony amefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kughushi cheti cha masomo ili kupata ajira ya umma.
Mashtaka dhidi ya Chepkwony yaliwasilishwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Tume hiyo ikisema uchunguzi wake ulibaini kuwa afisa huyo aliwasilisha cheti bandia cha mtihani wa kidato cha nne, KCSE akidai kilikuwa cha kweli kilichotolewa na Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini, (KNEC).
“Hii ilimwezesha kupata ajira kwenye kampuni hiyo ya maji na kisha kupata mshahara na mafao mengine ambayo kima chake ni shilingi milioni 7.59,” ilisema EACC kwenye taarifa.
Afisa huyo sasa anakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata mali ya umma kinyume cha sheria.
Hata hivyo, aliyakanusha mashtaka hayo alipofikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Milimani.
Chepkwony aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki moja pesa taslimu au dhamana mbadala ya shilingi nusu milioni.