Tume ya Maadili na kukabiliana na ufisadi Nchini (EACC), imepiga hatua baada ya mahakama kuamuagiza Jematia Kiptis ambaye ni afisa katika Hazina Kuu,kurejesha zaidi ya shilingi milioni 67 alizolipwa kinyume cha sheria kama marupurupu.
Kwenye uamuzi uliotolewa siku ya Jumatatu na Jaji Musyoki wa mahakama ya kushughulikia kesi za ufisadi Jijini Nairobi, mahakama ilibaini kuwa Kiptis alipokea kinyume cha sheria fedha hizo za umma ambazo zilibainika kuwa marupurupu bandia.
Mahakama hiyo ilimuagiza Faith Kiptis kurejesha shilingi milioni 67,664,975,huku shilingi milioni 2,443,667.92 zikinaswa kutoka akaunti yake kwenye benki ya Equity na shilingi milioni 6,320,419.80 kutoka akuanti yake ya benki ya KCB.
Kiptis pia atahitajika kulipia gharama ya kesi hiyo.
Maafisa wa uchunguzi wa EACC, waligundua kwamba kati ya mwezi Januari 2020 na Juni 2022, Kiptis alipokea marupurupu ambayo hayatambuliwi na miongozo ya Utumishi wa Umma.
Marupurupu hayo pia hayakuambatana na kiwango chake cha kazi na hayakuidhinishwa na Tume ya Kuratibu Mishahara na Marupurupu (SRC).
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za EACC ambazo zimesababisha kurejeshwa kwa shilingi milioni 174 zilizotolewa kwa njia haramu kwa maafisa wa Hazina Kuu.