Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi, EACC, jana Jumanne ilimkamata David Geoffrey Ombiro, afisa wa utawala katika bunge la kaunti ya Kisii kwa tuhuma za kutumia nyaraka zilizoguhushiwa kupata ajira.
Uchunguzi wa EACC ulibaini kuwa Ombiro alibadili cheti chake cha kuzaliwa, ambapo alibadili mwaka wake wa kuzaliwa kutoka 1967 hadi 1973, na alitumia cheti hicho kupata kitambulisho cha kitaifa kilichoakisi mabadiliko hayo.
Pia anatuhumiwa kwa kughushi Nambari Binafsi ya Utambulisho (PIN) ya Mamlaka ya Mapato (KRA), kadi ya Hazina ya Bima ya Taifa ya Afya (NHIF) na ile ya malipo ya uzeeni (NSSF) ili maelezo kwenye kadi hizo yawiane na yale yaliyopo kwenye cheti cha kuzaliwa.
Kisha aliwasilisha nyaraka hizo kwa bunge la kaunti ya Kisii kama sehemu ya rekodi zake za ajira.
EACC inasema baada ya kukamilisha uchunguzi wake, iliwasilisha faili ya kesi ya mtuhumiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ambaye aliidhinisha mashtaka dhidi ya mshukiwa.
Ombiro aliandikisha taarifa katika ofisi ya EACC ya kanda ya Nyanza Kusini na kisha kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kisii alikolala usiku kucha kabla ya kufikishwa katika mahakama ya kupambana na ufisadi ya Kisii leo Jumatano asubuhi.
Mshukiwa huyo alikana mashtaka dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 150,000 na mdhamini wa kiasi kama hicho au dhamana ya shilingi 70,000 pesa taslimu.
Kesi hiyo itatajwa Septemba 25 mwaka huu.