Utapiamlo umesababisha vifo vya watu wasiopungua 63, hasa wanawake na watoto, katika kipindi cha wiki moja tu katika mji uliozingirwa wa El-Fasher nchini Sudan.
Hii ni kwa mujibu wa afisa wa afya aliyezungumza na shirika la habari la AFP jana Jumapili.
Afisa huyo, aliyezungumza bila kutaka kutambulishwa, alisema idadi hiyo ilijumuisha tu wale walioweza kufika hospitalini.
Aliongeza kuwa familia nyingi ziliwazika wapendwa wao waliofariki bila kutafuta huduma za matibabu kutokana na ukosefu wa usalama na usafiri.
Tangu mwezi Mei mwaka jana, mji wa El-Fasher umezingirwa na vikosi vyenye hadhi ya kijeshi vya Rapid Support Forces (RSF), ambavyo vimekuwa vikipigana na jeshi la Sudan tangu mwezi Aprili mwaka 2023.
Mji huo unasalia kuwa mkubwa unaodhibitiwa na jeshi huko Darfur na katika siku a hivi karibuni umekabiliwa na mashambulizi mapya yaliyofanywa na RSF baada ya kundi hilo kuondoka katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum mapema mwaka huu.
Shambulizi kubwa la RSF katika kambi ya wakimbizi iliyo karibu ya Zamzam lilisababisha maelfu ya watu kukimbia tena, wengi wao ambao wametafuta hifadhi mjini El-Fasher.
Meko ya jamii yamefungwa kwa kiasi kikubwa kutokana na uhaba wa chakula. Baadhi ya familia zinasemekana kuishi kwa kula malisho ya wanyama au mabaki ya chakula.
Tkariban asilimia 40 ya watoto chini ya umri wa miaka 5 mjini El-Fasher kwa sasa wana kiwango kikubwa cha utapiamlo huku asillimia 11 wakikabiliwa na kiwango kikubwa zaidi cha utapiamlo, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa, UN.